Saturday, March 9, 2013

HILI NI ZAIDI YA SHAIRI KWAKO MJASIRIAMALI!!

From Malenga wa Mvita by Ahmad Nassir
UJANA
            

                    1
           Ewe ulo na busara, fikiri bibi na bwana,
           Fikiri lilo tohara, na lile lilo dhamana,
           Pia fikiri izara, wewe nayo kukutana,
           Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho

                    2
           Ujana ni jambo bora, ameupamba Rabana, 
           Tena umetia fora, ulitendalo hufana,
           Basi usiwe mkora, akiba uweke sana,
           Sihadawe na ujana na ujana una mwisho.

                    3
           Kuweka jambo dharura, jihimu kuweka mwana,
           Siyo pato kulipura, kwa usiku na mchana,
           Ukitoweka ujura, elewa umekubana,
           Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho.
          
                    4
           Hebu zituze fikara, ushike ninayonena, 
           Akiba kwako sitam, ukiijaza shehena,
           Na pia huwa kafara, na shida isije tena,
           Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho.
          
                    5
           Ufanyapo biashara, ewe kijana kazana, 
           Ujihimu kila mara, na akiba kushikana,
           Uzee ukikudara, uwe umetulizana,
           Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho.
           
                    6
           Kwa kweli Si masihara, mwanadamu hutatana,
           Kukosa kitu ni dhara, jina hutojulikana,
           Au uitwe fukara, mzee mja wa lana,
           Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho.
           
                     7
           Ujana hukuzingira, ukangiwa na fitina,
           Ukafikwa na majira, uzee ukawa jina,
           Basi na wako ujira. wa kazi weka hazina,
           Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho
 
AKIWA KAMA MSHAIRI ANAWEZA KUWATIA MOYO WENGINE,LAKINI PIA HII NI FURSA PEKEE 
KWAKE KUISHI KWAYO MAANA HATA KIPAJI NI MSINGI WA BIASHARA NA MATUNDA YA KIPAJI
 NDIO BIDHAA YENYEWE YA KUWAUUZIA WATEJA WAKO!

Yako mengi tu huku http://www.mwambao.com/mashairi.htm